Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MKANDARASI KAMA HAJAFIKISHA 60% YA KAZI ASIPEWE KAZI NYINGINE: BASHUNGWA


Waziri  wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kutowapa kazi nyingine Mandarasi ambao hawafikisha asilimia 60 ya kazi za awali ili kuondokana na  hali ya kumrundikia kazi za Ujenzi mkandarasi mmoja.

Amesema hayo tarehe 09 Oktaoba 2023 wakati akiongea na Wananchi wa kijiji cha Isenyi wilaya Serengeti mkoani Mara wakati wa ziara ya ukaguzi, utekelezaji wa miradi inayotekelezwa mkoani Mara.

"Nawaagiza TANROADS, Kama kuna Makandarasi wanaotekeleza Barabara au kazi nyingine ya Ujenzi na wako chini ya asilimia 60 ya utekelezaji, msiwape miradi mingine mipya” amesisitiza Bashungwa

Aidha, Bashungwa hajaridhishwa na utekelezaji wa  Barabara ya Sanzate - Nata unaotekelezwa na Kampuni ya China Railway Seven Group wenye urefu wa kilometa 40 ambapo utekelezaji huo unasuasua kwa miaka mitatu kwa sababu ya kurundikiwa kazi nyingi za Ujenzi.

Amesema Mkandarasi huyo ana miradi minne ambayo ni Sanzate- Nata km 40, Kibaoni – Stalike, mradi wa Sanifu na Jenga, mradi wa Barabara ya Kibaoni – Mlele (km 50), mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Amanimakoro – Ruanda (km 35), mradi wa ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Nyamwage - Utete (km 33.7) na ujenzi wa Daraja la Mpiji Chini.

Ili kuhakikisha mradi huo unakamilika, Waziri Bashungwa amemuagiza Mkurugenzi wa Barabara Wizara ya Ujenzi, Mhandisi Aloyce Matei na Mkurugenzi wa Miradi TANROADS Mhandisi Boniface Mkumbo kuhakikisha wanarudi Mkoani Mara baada ya ziara ili kusimamia kikamilifu mradi huo.

Bashungwa amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaelewa Mkoa wa Mara unachangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kwa kuwa na asilimia 75 ya mbuga ya Serengeti na kushika namba mbili kwa uzalishaji wa dhahabu nchini.

Awali akitoa taarifa ya mradi, Mhandisi Boniface Mkumbo amesema kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 41 na tayari Mkandarasi amelipwa Shilingi bilioni 19.4 ikiwa ni malipo ya hati za madai pamoja na malipo ya awali ya Shilingi bilioni 5.7

Mkumbo amesema kuwa Shilingi milioni 978 zimelipwa fidia ya mali na ardhi kwa mujibu wa sheria kwa wananchi 291 walioathiriwa na mradi.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo umezalisha jumla ya ajira 172, kati ya hizo ajira 159 ni Watanzania sawa na asilimia 92.4 ya ajira zote.

Barabara ya Sanzate - Natta yenye urefu wa km 40 ni sehemu ya barabara ya kutoka Musoma hadi Arusha kupitia mbuga za wanyama za Serengeti na Ngorongoro, Mto wa Mbu hadi Arusha na pia ni kiungo muhimu kati ya mikoa ya Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kaskazini pamoja na nchi jirani ya Kenya.