Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MIUNDOMBINU YA BARABARA MTWARA INAENDELEA KUIMARISHWA: RAIS SAMIA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara zinazounganisha Wilaya zote za mkoa wa Mtwara  ili kurahisisha usafirishaji wa mazao.

Ameyasema hayo Septemba 17,2023 katika mkutano wa hadhara uliofanyika Masasi mkoani Mtwara wakati anahitishisha ziara mkoa huo na kuendelea na ziara Lindi.

“Barabara ya Mtwara -Tandahimba- Newala- Masasi ambapo kwa sasa kilometa 50 zimekamilika lakini kilometa 160 zilizobaki kuna wakandarasi wawili wataingia kazini hivi karibuni ili kuijenga barabara hii mpaka Masasi”. amesema Rais Samia 

Aidha, Rais Dkt. Samia amesema zipo barabara zilizoombwa na kwa umuhimu wake Serikali imechukua barabara ya Masasi - Nachingwea- Liwale ambayo ni Kilometa 175, mkataba tayari umeshasainiwa na upo katika hatua za mwisho za kutafuta fedha ili barabara hiyo ianze kujengwa.

“Zile nyingine zitakwenda kujengwa kama alivyosema Waziri wa TAMISEMI kupitia TARURA zitakwenda kujengwa kama nilivyoagiza”- amesisitiza Rais Dkt.Samia

Kuhusu Taa za Barabarani, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali imetenga Shilingi Bilioni 1.3 kuweka taa za barabarani katika maeneo ya Mangaka, Masasi na Nanyumbu ambapo taa hizo zinawekwa hivi karibuni kwani fedha yake ipo.