Habari
MAKANDARASI WAZAWA KUPEWA MIRADI HADI YENYE THAMANI YA BILIONI 50: BASHUNGWA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Fedha imesikia kilio cha Makandarasi Wazawa na imeamua kupandisha wigo wa thamani ya miradi kwa Makandarasi hao kutoka kiasi cha Shilingi Bilioni 10 hadi kufikia Shilingi Bilioni 50.
Ameeleza kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara imetenga jumla ya kilometa 120 kwa ajili ya kutekelezwa na Makandarasi Wazawa ukilinganisha na kilometa 102 zilizotekelezwa na Wakandarasi hao kwa kipindi cha miaka 11 iliyopita.
Bashungwa ameeleza hayo Bungeni jijini Dodoma leo Juni 26, 2024 wakati akichangia Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2024/2025 na kumshukuru Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba kwa kurekebisha Sheria ya Manunuzi na Kanuni zilizokuwa pingamizi za ushiriki wa Makandarasi Wazawa katika utekelezaji wa miradi nchini.
“Sasa hivi thamani ya miradi imepanda hadi Bilioni 50 na baada ya Bajeti hii Wizara ya Ujenzi kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) tutajipanga na kuhakikisha kanuni hii inaanza kutekelezwa ipasavyo kwa mwaka 2024/2025”, ameeleza Bashungwa.
Aidha, Bashungwa ameongeza kuwa Wizara inaendelea na mazungumzo na wafadhili wa mashirika ya maendeleo ikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika kuruhusu kipengele cha ‘Sub Contracted’ kwa ajili ya Makandarasi Wazawa katika miradi mikubwa inayotekelezwa ili kuweza kuwainua makandarasi nchini.
Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa Wizara imefanya marekebisho katika upande wa manunuzi ya kumtafuta mzabuni katika miradi ya TANROADS ambayo imekuwa ikikwamisha Makandarasi Wazawa bila sababu za msingi na kusisitiza utekelezaji wake kuanza Mwezi Julai, 2024.
Amesema kuwa Serikali inaendelea na mazungumzo na mabenki ili kuona namna ya kuwasaidia Makandarasi Wazawa kuanza kazi bila kuchelewa kwa kupata malipo ya Awali wakati Serikali ikiendelea kushughulikia malipo yao.