Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

MAJALIWA AWATAKA ERB KUJA NA MKAKATI WA KUWAINUA WAHANDISI WA NDANI


Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameitaka Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), kupeleka mapendekezo Serikalini ya namna ya kuwatumia wahandisi wa ndani katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ili kuwapa fursa ya kukua na kuongeza uzoefu katika miradi hiyo.

Akifungua mkutano wa 20 wa siku ya wahandisi nchini Waziri Mkuu Majaliwa amesema dhamira ya Serikali ni kuona sekta ya uhandisi nchini inakuwa na kuwapa fursa wahandisi wazawa ambao mchango wao katika maendeleo ya nchi ni mkubwa.

“Hakikisheni mnaungana, mnakopa katika benki ili muwe na nguvu ya  kutekeleza miradi mingi inayoendelea kutekelezwa na serikali hususan ya ujenzi wa miundombinu”, amesema Mhe. Majaliwa.

Aidha, amewataka wahandisi hao kutumia fursa kwa kuwa wabunifu na kuendana na teknolojia  ili nchi isibaki nyuma katika kuchagiza maendeleo katika sekta ya miundombinu, sayansi na teknolojia.

“Tumieni vizuri siku hizi mbili kufanya uchambuzi wa kina na kuja na mapendekezo yatakayowezesha Serikali kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuwawezesha kushiriki katika ujenzi wa miradi mikubwa inayoendelea nchini”, amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Ameutaka Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), kuwapatia wazawa miradi midogo inayoendelea ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa katika siku zijazo kama inavyofanya TANROADS.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ujenzi Mhandisi, Godfrey Kasekenya amesema Serikali inatambua umuhimu wa wahandisi katika kuleta maendeleo ya taifa ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imetenga shilingi milioni 726, kwaajili ya mradi wa SEAP – mradi ambapo umelenga kuwajengea wahitimu wa fani hiyo uzoefu.

Aidha katika kuchochea wanawake kufanya shughuli za kihandisi Mhandisi Kasekenya amesema Wizara imetenga miradi maalum ya ujenzi wa barabara kwaajili ya kuwawezesha wahandisi wanawake kutekeleza miradi hiyo ili kuwajengea uwezo.

Kwa upande wake Mweyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi, Menye Manga amewataka wahandisi kufanya kazi kwa weledi kulingana na viapo vyao kutokana na umuhimu wa kada hiyo kwa maslahi ya taifa na  umma kwa ujumla.

Naye Msajili wa ERB Mhandisi,Bernard Kavishe amesema mpaka sasa Bodi hiyo imesajili wahandisi 36,706. ambapo kati ya hao wahandisi wanawake ikiwa ni 4,653 sawa 13%.

Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika jijini Dare es Salaam pamoja na mambo mengine utajadili fursa za kihandisi na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoikabili sekta hiyo.