Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

Magari kupita daraja jipya la Selander Desemba


Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, amesema ujenzi wa Daraja  jipya la Selander lililopo jijini Dar es Salaam lenye urefu wa km. 1.03 na upana wa mita 20.5 ujenzi wake umefikia asilimia 93, kwamba  linatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu,

Daraja hilo lenye barabara unganishi zenye urefu wa km 5.2 linajengwa na Kampuni ya GS Engineering ya Korea, litakalopita baharini kuanzia ufukwe wa Coco Beach (Oysterbay) kwenda Hospitali ya Aga Khan (Maeneo ya Ocean Road).

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya  mradi huo, Waziri Mbarawa alisema hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 93 na kwa sasa mkandarasi anaendelea na ujenzi wa sehemu  ya juu ya daraja baada ya kukamilisha ujenzi wa sehenu ya chini kwa asilimia 100 ikiwamo, nguzo za msingi 254, vitako vyake 16  pamoja na nguzo 16 za juu za daraja.

"Mkandarasi amekamilisha kujenga km 1.026 kati ya km 1.030 sawa na asilimia 99.7 na kuweka nyaya za daraja 30 kati ya 30 sawa na asilimia 100," alisema Prof. Mbarawa.

Aliongeza kuwa kwa upande wa barabara unganishi mkandarasi anaendelea na kazi za kukamilisha ujenzi wa Barabara ya Barack Obama, Toure, na barabara mpya zenye upana sawa na ule wa daraja.

Aidha, akiwa katika ukaguzi huo Profesa  Mbarawa aliridhishwa na ushirikishwaji wa wazawa kwenye mradi  mbapo jumla ya wafanyakazi 773 kati ya hao wafanyakazi 704 ni wazawa sawa na asilimia 9I.

"Nimefurahishwa sana kukuta wataalamu wanaojenga mradi huu ni Watanzania na ninategemea mafunzo haya yatasaidia kujenga uwezo na ujuzi utakaosaidia taifa letu baadae," alisema Prof. Mbarawa.

Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Mativila, akiwasilisha taarifa ya mradi alimueleza Waziri Mbarawa kwamba kazi zinazoendelea kwa sasa upande wa barabara ni ujenzi wa tabaka la mwisho la lami, ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua pamoja na uwekaji nguzo za taa na misingi yake pamoja na usimikaji wa taa za barabarani.

Mhandisi Mativila ameongeza kuwa wanatarajia ifikapo mwishoni mwa Desemba mwaka huu kazi ndogo ndogo zitakuwa zimekamilika na kuanza kupitisha magari kwa majaribio.

Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi jijini Dar es Salaam ambapo amekagua ujenzi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa chini ya wizara yake ikiwemo upanuzi wa gati namba moja hadi  saba katika Bandari ya Dar es Salaam, upanuzi wa Barabara ya Kimara hadi Kibaha, ujenzi wa Daraja jipya la Selander pamoja na  Mradi wa Ujenzi wa miundombinu ya Mabasi yaendayo Haraka (BRT) awamu ya pili.