Habari
KASEKENYA AAGIZA KUWEKWA ALAMA ZA TAHADHARI MLIMA BUSUNZU
Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na Mkandarasi STECOL kuhakikisha wanaweka alama za tahadhari na kukagua mara kwa mara eneo la Mlima Busunzu sehemu ilipotokea changamoto ya kuharibika kwa kipande cha barabara chenye urefu wa takriban mita 100, wakati wakisubiri utatuzi wa kudumu kwenye eneo hilo.
Kasekenya ameelekeza hayo wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Kabingo- Kasulu- Manyovu (Km 260), sehemu ya Mvugwe - Nduta (Km 59.35) na kueleza kuwa mkandarasi bado yupo eneo la mradi na kwa sasa anasubiri timu ya wataalamu inayofanya utafiti kuhusu kupata ufumbuzi wa tatizo hilo ili kuendelea na ujenzi katika kipande hicho.
"Hakikisheni mnaendelea kuliangalia eneo hili, hata barabara zinazopita katika eneo hili zikagueni mara kwa mara na muweke alama za tahadhari ili watu wanapopita hapa wapite kwa uangalifu," amesema Kasekenya.
Aidha, Kasekenya ameongeza kuwa Serikali inaendelea na Ujenzi wa barabara ya Manyovu - Mnanila - Kasulu ambapo zaidi ya Kilometa 26 za barabara hiyo zimewekwa lami na inatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba mwaka huu.
Kadhalika, Kasekenya ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuufungua Mkoa wa Kigoma na nchi kwa ujumla kupitia Miundombinu ya barabara na hivyo kurahisisha huduma za usafiri na usafirishaji kati ya Mkoa huo na Mikoa jirani ya Geita, Mwanza pamoja na nchi jirani za Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Kasekenya, amemuelekeza Meneja wa TANROADS Mkoa huo kuendelea kuwasimiamia wakandarasi wanaojenga barabara hizo kukamilisha kwa wakati na kwa ubora ili kusaidia wananchi kuondokana na changamoto wanazozipata hususan kipindi cha mvua.
Kwa upande Wake, Mhandisi, Hamisi Juma kutoka Kampuni ya Mhandisi Mshauri M/s Conseil Ingenierie Limited (CIRA SAS) amesema kwa sasa mradi umefika asilimia 81.49 ambapo tabaka la lami limeshawekwa mpaka mwisho wa mradi na unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti, 2024.
Mhandisi, Juma ameongeza kuwa ujenzi wa mradi huo umehusisha pia na Ujenzi wa daraja la Malagarasi lenye urefu wa mita 77 na madaraja mengine mawili ambayo yote yamekamilika kwa asilimia 100.
Mradi wa barabara ya Mvugwe- Nduta (Km 59.35) umefadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na unagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 84.