Habari
KADOGOSA: FOLENI DAR ZITAFUTIWE SULUHISHO LA HARAKA
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, ameiagiza TANROADS kuimarisha mikakati ya kupunguza foleni katika Jiji la Dar es Salaam kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.
Agizo hilo amelitoa leo, Oktoba 8, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati alipokutana na Mameneja wa TANROADS wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara na Morogoro na kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi pamoja na maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Nino.
Kadogosa amesema TANROADS inapaswa kuongeza kasi katika kutafuta suluhisho la foleni, ikiwemo kudhibiti magari yanayopaki hovyo barabarani.
“Sifurahishwi na namna ambavyo magari yanavyopaki hovyo barabarani. Msongamano ni mkubwa na unasababisha kero kwa watumiaji wengine wa barabara,” amesema.
Aidha, ameitaka TANROADS kukamilisha mapema maandalizi ya kukabiliana na athari za mvua za El Nino, hususan katika maeneo hatarishi kwa kupeleka vifaa vya kuchukua tahadhari Pamoja na kufanya maboresho katika Makalvati na madaraja yaliyoziba.
Waziri Kadogosa yupo jijini humo, kwa ajili ya mwendelezo wa Vikao vyake vya kukutana na Mameneja wa TANROADS katika mikoa mbalimbali nchini kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi katika mikoa hiyo na kupokea mikakati ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha nchini.
