Habari
KADOGOSA AWATAKA WATUMISHI WIZARA YA UJENZI KUSHIRIKIANA KUFIKIA MALENGO YA SERIKALI
Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, amewataka watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kufanya kazi kwa ushirikiano, ubunifu na weledi ili kufanikisha malengo na matarajio ya Serikali kupitia wizara hiyo.
Waziri Kadogosa ametoa agizo hilo mkoani Arusha, wakati akizungumza na watumishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi zinazotekeleza majukumu mbalimbali mkoani humo.
Amesema ushirikiano miongoni mwa watumishi katika taasisi ni muhimu katika kuhakikisha majukumu yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyowekwa na Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi.
Aidha, Waziri Kadogosa amewataka watumishi hao kuongeza ubunifu na kufanya kazi kwa weledi ili kuongeza tija na ufanisi katika taasisi zao, hatua ambayo itachangia katika kuleta maendeleo ya Sekta ya Ujenzi na Taifa kwa ujumla.
Katika kikao hicho, Waziri Kadogosa amezungumza na watumishi kutoka taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi, zikiwemo Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Vikosi vya Ujenzi pamoja na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).
