Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

JENGO LA WIZARA YA UJENZI NA UCHUKUZI, MTUMBA KUKAMILIKA DISEMBA


Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Eng. Godfrey Kasekenya amezitaka Taasisi za Vikosi vya Ujenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wanaojenga na kusimamia ujenzi wa jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi katika Mji wa Serikali, Mtumba, jijini Dodoma kuhakikisha jengo hilo linakamilika katika ubora uliokusudiwa ifikapo Disemba mwaka huu.

 Amesema licha ya kujenga majengo mazuri taasisi hizo ziwe mfano wa upandaji miti na utunzaji wa mazingira katika miradi yote inayotekelezwa na taasisi hiyo ili kulinda mazingira na kuboresha mandhari.

“Kazi yenu ni nzuri na hatua mliyofikia ya asilimia 68 inatia moyo, Serikali itahakikisha malipo yanafanyika kwa haraka ili kuwawezesha kuagiza vifaa na kuvifunga kwa wakati na hivyo kuendana na ratiba ya kukamilisha majengo hayo”, amesema Naibu Waziri Kasekenya

Amezungumzia umuhimu wa taasisi hizo zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kuhakikisha miradi yote ya ujenzi inayoisimamia inakamilika kwa wakati na kwa ubunifu.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Vikosi vya Ujenzi Eng.Simeoni Machibya, amemhakikishia Naibu Waziri huyo kuwa miradi yote waliyokasimiwa kuijenga itakamilika kwa wakati na hivyo kufikia malengo makubwa ya Serikali.

“Tumejipanga kuhakikisha kuwa majengo ya wizara ya Tamisemi, Mambo ya Nje na Ujenzi na Uchukuzi yanakamilika ifikapo Disemba na yanapendeza kutokana na kupandwa miti na maua ili kutunza mazingira”, amesisitiza Eng Machibya.

Msimamizi wa mradi huo Arch.Weja Ng’olo kutoka TBA amesema ujenzi wa jengo la wizara umefikia asilimia 68 na kazi inayoendelea ni ya ukamilishaji na ufungaji wa miundombinu ya ndani na ya jengo na kujenga uzio na atahakikisha jengo la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi linakuwa la mfano kwa kukamilika kwa muda na ubora unaotakiwa.

Zaidi ya shilingi bil.28 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo ambao ni sehemu ya majengo 27 ya mji wa Serikali yanayojengwa Mtumba, jijini Dodoma.