Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

FURSA NA MITAJI SEKTA YA UJENZI INAKUJA, KIKUBWA TUWAJIBIKE; WAZIRI BASHUNGWA.



Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kutafuta fedha kupitia wahisani mbalimbali wa maendeleo ili kusaidia Makandarasi wa ndani kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi mbalimbali ya miundombinu nchini.


Akiongea kupitia kipindi cha Mizani ya Wiki cha U TV, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa Serikali  kupitia Wizara ya Ujenzi imeshakaa na baadhi ya Benki na wadau mbalimbali wa maendeleo kuona namna ya kusaidia kuwezesha Makandarasi wa ndani katika  kutafuta fursa mbalimbali kupitia Sekta ya Ujenzi.


"Tutatengeneza fursa ambazo zitakuwa rafiki kwa Makandarasi wetu ili washiriki kikamilifu katika miradi ya kuijenga na kukarabati nchi yetu" ameeleza Bashungwa.


Bashungwa amebainisha kuwa Serikali itatoa  kipaumbele kwa Makandarasi wa ndani na kusisitiza  makandarasi hao kufanya kazi  kwa viwango na kufuata mikataba.


Amefafanua kuwa katika utekelezaji wa miradi Serikali itaangalia uzoefu wa wataalam badala ya kampuni ili kuhakikisha kila Mkandarasi anayepewa kazi ana uwezo binafsi wa kusaidia usimamizi na ujenzi wa miradi yetu.
 

Ameeleza kuwa Mpango wa Wizara kwa siku za usoni ni kuchukua Wahandisi waliomaliza vyuo vikuu ili wasajiliwe ERB na kuwapeleka mafunzo ya vitendo  kwa muda wa miaka 3 kwenye miradi mbalimbali ili baadae wajiunge katika vikundi na kupata miradi midogomidogo ili  wakue kiujuzi na utaalam na hapo baadae Serikali itaangalia namna ya kuwaanzishia mifuko ya kuwasaidia ili waendelee kujiimarisha na kutodumaza taaluma zao.