Habari
BASHUNGWA AUNDA KAMATI YA KUPITIA MIFUMO YA TEMESA
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema ameunda kamati kwa ajili ya kupatia ufumbuzi wa uboreshaji wa karakana zote za Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), ili kuusaidia Wakala huo uweze kufanya kazi kwa ufanisi na kuleta tija inayokusudiwa kwa jamii na Serikali.
Bashungwa amezungumza hayo mkoani Morogoro mara baada ya kupokea changamoto za Madereva wa Serikali katika Kongamano la 2 la Chama cha Madereva Serikali ambapo wameomba liangaliwe upya suala la Sheria ya Manunuzi ya Umma ambayo inawapa uhalali TEMESA kutumia gharama kubwa zaidi ya bei ya soko za matengenezo ya magari ya Serikali pamoja na ufungaji wa vipuri feki.
Bashungwa amewatoa wasiwasi madereva hao pamoja na wadau wote wa Wakala huo ambapo tayari Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekwishatoa maelekezo ya changamoto hizo na utendaji kazi wa karakana zote za TEMESA ili kuisaidia kutoa huduma bora.
Aidha, Bashungwa amesema Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi imeanza kuchukua hatua ya kuboresha karakana za TEMESA na kutumia tekenolojia za kisasa katika mifumo yao kwa kuanzisha ubia na kampuni ya TOYOTA.
Bashungwa amebainisha changamoto alizozikuta katika baadhi ya karakana za TEMESA ikiwemo ya mfumo wa zamani wa kupokea na kutoa vipuri stoo ambayo hupelekea udanganyifu wa mafundi wasio waaminifu kwa kubadilisha vipuri halisi na vipuri feki.
“Nilipotembelea baadhi ya karakana na nilikuta mifumo ya zamani ya upokeaji wa vifaa wakati hivi sasa kuna teknolojia ya namba ya utambulisho (barcode) ambayo inarahisha utambuzi wa aina gani ya vipuri vilivyoingia na kutoka? tarehe gani? na mhusika aliyepokea”, amesema Bashungwa.
Sambamba na hilo, amesema wamejipanga kuhakikisha magari yakifika TEMESA yanatengenezwa haraka na kwa ubora ambao hautasababisha gari kurejeshwa kwa matengenezo hayo hayo ili kuvutia wadau wetu na kuongeza wateja wengine.