Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AKERWA NA KASI NDOGO UJENZI WA MSALATO AIRPORT


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza kampuni ya Beijing Construction Engineering Group kuhakikisha inakamilisha ujenzi wa jengo la abiria na jengo la kuogozea ndege katika Kiwanja cha Kimataifa cha Msalato, Dodoma ifikapo Desemba, 2024 kulingana na maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Bashungwa amesema hayo leo Septemba 28, 2023 jijini Dodoma wakati akikagua maendeleo ya ujenzi wa kiwanja hicho na kutokuridhishwa na kasi ya maendeleo yake kutokana na kusuasua kwa mkandarasi huyo.

"Mkandarasi usivimbe kichwa kana kwamba umepata kazi nyingi, usipozingatia maelekezo ambayo nimekupatia, kulingana na vipengele vilivyopo kwenye mkataba, tunaweza kukusimamisha kazi kwa mujibu wa sheria", amesema Bashungwa.

Amemtahadharisha Mkandarasi huyo iwapo atazembea kukamilisha kazi hiyo kwa wakati itampelekea kutopata kazi nyingine katika Sekta ya Ujenzi ndani ya nchi.

“Ukizembea kwenye kazi hizi, nina mamalaka ya kuhakikisha hupati kazi nyingine ndani ya nchi hii, baada ya ziara hii nataka kuona kazi inaenda kwa spidi”, amesisitiza Bashungwa.   

Aidha, Bashungwa amemtaka Meneja Mkazi wa Kampuni hiyo kuripoti ofisini kwake na kumuandikia maelezo ya mpango kazi wake na ‘commitment letter’ ya kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Ameelekeza msimamizi wa miradi kutoka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) kahakikisha anasimamia mradi huo masaa 24 ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa ubora na kwa wakati kama ilivyopangwa.

Bashungwa amebainisha kuwa ujenzi wa jengo hilo unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo sehemu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua kwa ndege yenye urefu km 3.6, maegesho ya ndege, Tax way, barabara za maingilio ambapo hadi sasa utekelezaji wake ni asilimia 36 huku, sehemu ya pili inahusisha ujenzi wa jengo la abiria pamoja na jengo la kuongozea ndege na miundombinu mengine ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 7.

Awali wakati akikagua barababara ya kuruka na kutua ndege, Bashungwa amempongeza mkandarasi Sinohydro Corporation anayeshirikiana na M/s Beijing Sino – Aero Construction Engineering na M/s China Jiangxi International Economic and Technical Cooperation kwa kuendelea kutekeleza mradi huo na kumsisitiza kuendelea kufanya kazi usiku na mchana ili uweze kumalizika kwa wakati.

Akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Eng. Mohamed Besta amesema kuwa watahakikisha wanawasimamia wakandarasi wote wawili wanaojenga Kiwanja hicho ili kumalizika ndani ya muda kwa kuweka sawa ratiba yao ili iendane na muda waliopangiwa na kupata matokeo yanayoyatarajia.

Ukamilikaji wa kiwanja hicho ambacho sehemu ya kwanza ya ujenzi wake inagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 165 ni moja ya mkakati wa Serikali katika kuboresha na kuimarisha usafiri wa anga, ambapo kiwanja hicho kitakuwa na uwezo wa kupokea abiria Milioni 1.5 kwa mwaka na abiria 800 kwa wakati mmoja.