Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA ABAINISHA MIKAKATI YA SERIKALI YA KUINUA KADA YA MADEREVA SERIKALINI.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali imekwishafanyia kazi maboresho ngazi ya miundo ya Madereva wa Serikali na kuondoa vigezo ambavyo hapo awali vilikuwa vinakwamisha kada hiyo kupandishwa vyeo na madaraja. 

Bashungwa ameyasema hayo mkoani Morogoro wakati akimkaribisha mgeni rasmi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kufungua Kongamano la pili la Chama cha Madereva wa Serikali Tanzania ambalo limebeba kauli mbiu ya "Dereva wa Serikali Bila Ajali Inawezekana". 

"Wizara ya Ujenzi ndio msimamizi mkuu wa kada ya madereva hivyo Serikali imeanza kufanyia kazi utekelezaji wa miundo mipya ya kada hii na rasmi imeanza kutekeleza mnamo tarehe 01 Juni, 2023", amefafanua Bashungwa. 

Amesema maboresho hayo yaliyoridiwa na Ofisi ya Rais (UTUMISHI) yakiwemo ya kubadilisha muundo wa kada hiyo kutoka TGOS kwenda TGS, kuondoa kikwazo cha kuhitaji sifa ya cheti cha majaribio ya ufundi na kubadlishiwa masharti ya kazi kutoka ya kawaida hadi ya Kudumu na Malipo ya Uzeeni. 

Amesema kuwa Wizara yake inaendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye anasisitiza Serikali kuzingatia maoni ya watumishi wa kila kada ili kuhakikisha kwamba utendaji kazi unaleta tija na ufanisi kwa kuzingatia dhana ya mazingira wezeshi Serikalini. 

Aidha, Bashungwa ameiwaagiza Madereva wa Serikali kutekeleza kazi zao kwa weledi, uadilifu, uzalendo na kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani. 

"Jamii imekuwa ikiwanyooshea vidole baadhi yenu (madereva wa Serikali), kwa kutokuzingatia ipasavyo masuala ya usalama barabarani hivyo mbadilike na muwe wa mifano ya kuigwa" amesisitiza Bashungwa. 

Bashungwa amewakumbusha madereva kutojihusisha kwenye vitendo vya ukiukwaji wa maadili ikiwemo kutumia vilevi ambavyo vitaathiri afya zao pamoja na utekelezaji wa majukumu yao ambayo yanabeba dhamana ya uhai na maisha ya binadamu. 

"Niwaase kuzilinda afya zenu ili kujiepusha kupata magonjwa yanayoambukiza na yasiyoambukiza", amefafanua Bashungwa. 

Naye, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Charles Mwaihojo ameeleza kuwa kongamano hilo limehudhuriwa madereva 550 kutoka mikoa yote Tanzania ukilinganisha na kongamano la kwanza lililokuwa na wananchama 300. 

Ameeleza kuwa kongamano litakuwa na mafunzo mbalimbali yanayohusu masuala ya Utumishi wa Umma, Elimu ya Afya, Mikopo, Teknolojia ya magari ya kisasa, Mifuko ya Pensheni na mengine mengi. 

Chama cha Madereva Serikali Tanzania kilianzishwa mwezi Julai 07, 2013 na kupata usajili wake mwezi Septemba 15, 2015 ambapo hadi sasa kina wanachama wapatao 5,973.