Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AAGIZA WAHANDISI KUJENGEWA UWEZO.


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameiagiza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kuiwezesha na kuiendeleza taaluma ya kihandisi ili kuongeza ushindani katika Soko la ndani na nje ya nchi.

Waziri Bashungwa ameyasema  hayo  jijini Dodoma mara baada ya kuzindua jengo jipya la Bodi hiyo “Mhandisi Annex” ambalo limejengwa na wahandisi wazawa.

Bashungwa amesema kuwa Serikali bado ina uhitaji mkubwa wa wahandisi kwani Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anahakikisha anaifungua nchi kutokana na uwekezaji mbalimbali anaofanya kupitia miradi mbalimbali, kwa namna moja ama nyingine wahandisi wanahitajika kwa wingi ili kutekeleza miradi hiyo.

“ERB muendelee kusimamia taaluma hii, Watanzania tunaitegemea katika kuendeleza nchi yetu, tuijenge nchi yetu katika namna ambayo mchango wa Mhandisi utaonekana katika kuifanya Tanzania ipendeze na kuwa sehemu ya kuigwa”, amesema Bashungwa.

Bashungwa ameiagiza Bodi hiyo kuhakikisha inaandaa mpango mkakati wa kuwajengea uwezo wataalamu wake ili waweze kutekeleza miradi hiyo na kuweza kuleta tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Aidha, ameiagiza Bodi hiyo kuendelea kuiheshimu na kuitendea haki taaluma hiyo kwa kuhakikisha miradi wanayoitekeleza inakuwa bora na yenye viwango.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Eng. Menye Manga, ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo ya Waziri huyo ambapo amesema kuwa watahakikisha wanafuata, sheria, kanuni na taratibu katika kutekeleza majukumu yao.