Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BASHUNGWA AAGIZA TATHIMINI UJENZI WA MIZANI


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza wataalam wa wizara hiyo kufanya tathimini ya mizani zote nchini na kuangalia bajeti ya kuweka mizani ya kigitali ya kupima uzito wa magari yakiwa kwenye mwendo (weigh in motion), ili iwe katika vipaumbele vya Serikali katika mizani zote ambazo hazijafungwa mfumo huo na zile zitakazojengwa.

Bashungwa ameyasema hayo Oktoba 3, 2023 mkoani Mbeya wakati akikagua kazi zinazoendelea katika mzani wa Uyole uliopo mwanzoni mwa barabara ya Uyole - Kasumulu (mpakani mwa Tanzania na Malawi).

"Dhamira ya Serikali ya kujenga mizani hizo nchini sio kutoza tozo bali ni kujenga utamaduni wa kutozidisha uzito ili kulinda barabara hizo", amesema Bashungwa.

Ameongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu ametoa fedha ya ujenzi wa barabara kuwa njia nne ili kupunguza foleni katika barabara hiyo hivyo ni vema na mizani zitakazokuwepo ziendane na barabara hiyo.

Aidha, Bashungwa ametoa wito wa wasafirishaji wote nchini kuendelea kuzingatia viwango vya uzito vilivyotolewa kwa ajili ya kutumia barabara zetu ili kuendelea kuzilinda barabara na kuepuka kuingia gharama za tozo za kuzidisha uzito.

Naye, Mkurugenzi wa Miradi kutoka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Eng. Boniface Mkumbo amesema mzani huo unasaidia kudhibiti magari ya mizigo na ya abiria yanaoenda /yanaotoka Malawi, Kyela na Rungwe.

Ameongeza kuwa katika Mkoa wa Mbeya kuna mizani miwili ambayo ni Uyole na Mbugani  ambayo inatumika kwa udhibiti wa uzito wa magari.

"Mzani wa Uyole unapima mitarimbo kwa pamoja mitarimbo mitatu (Group Axle Weigher) wakati Mzani wa Mbugani (Chunya) unapima mtarimbo mmoja mmoja (Single Axle weigher)", amefafanua Eng. Mkumbo.

Mtandao wa Barabara unaosimamiwa na TANROADS una jumla ya mizani 76 ya Kudumu na inayofanya kazi ambapo kati ya hiyo mizani 58 haijawekwa mfumo wa kupima magari yakiwa kwenye mwendo (WIM) na 15 imeshafungwa tayari ambayo ni Vigwaza North na Vigwaza South (Pwani), Mpemba (Songwe), Nala (Dodoma), Mikese South (Morogoro), Wenda North na Wenda South (Iringa), Njuki (Singida), Dakawa North na Dakawa South (Morogoro), Kimokouwa East na Kimokouwa West (Arusha).