Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

BARABARA YA USHIROMBO - KATORO KUANZA KUPINGWA LAMI: BASHUNGWA


Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Wakala ya Barabara (TANROADS) imekamilisha Usanifu wa Barabara ya Ushirombo - Nyikonga - Katoro na Sasa Serikali ipo katika hatua ya kumtafuta Mkandarasi wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kipande cha Ushirombo hadi Nyikonga (km 22.5), pamoja ujenzi wa Daraja la Nyikonga.

Bashungwa ameeleza hayo leo tarehe 08 Juni 2024 katika Mkutano wa hadhara wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Bukombe, Dkt. Dotto Biteko katika Kata ya Katome Mkoani Geita.

“Tumeshakamilisha usanifu barabara ya Ushirombo - Nyikonga - Katoro, sasa tunaenda kumtafuta Mkandarasi kuanza ujenzi kuanzia Ushirombo hadi Nyikonga kilometa 22.5 na baada ya hapo tutamalizia kipande kilichobaki mpaka Kataro” ameeleza Bashungwa.

Ameeleza kuwa Serikali imeshapata Mkandarasi wa kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami Barabara ya Kahama - Bulyanhuru - Bukoli hadi Geita Mjini kwa kuanza ujenzi kipande cha Kahama hadi Bukoli.

Aidha, Waziri Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuiunganisha Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa kuboresha miundombinu ya barabara ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo - Busisi) Kilometa 3.2 pamoja na barabara unganishi ya Kilometa 1.66, linalounganisha Mkoa wa Mwanza na Geita ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 89.

“Tunamshukuru Mheshimwa Rais, Dkt. Samia Sukuhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za ujenzi wa Daraja la J.P Magufuli (Kigongo - Busisi) ambalo limefikia asilimia 89 na litakamilika mwezi Disemba mwaka huu na kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa wananchi wa Mikoa ya Kanda ya Ziwa” amesisitiza Bashungwa.

Amesema katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/25, Serikali imetenga fedha ya kuanza upanuzi wa njia nne barabara kuanzia Mwanza Mjini -  Nyegezi - Usagara mpaka Busisi katika Daraja la J.P Magufuli ili kuondoa changamoto ya foleni ya magari katika barabara hiyo.
 

Kadhalika, Bashungwa amesema kuwa Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ufungaji wa taa za barabarani katika Mitaa ya Mji wa Bukombe ili upendeze na kutoa fursa kwa wajasiliamali kuendelea kufanya biashara mpaka usiku.