Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Ujenzi

Habari

AQRB YAAGIZWA KUONGEZA MAPATO


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu imeielekeza Bodi ya Usajili ya Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) kuhakikisha wanaongeza vyanzo vya mapato ili kuweza kuongeza Bajeti yao na kufikia malengo waliojiwekea.

Akizungumza mara baaada ya kupokea Taarifa ya Utendaji wa Bodi hiyo, leo Tarehe 17 Oktoba, 2023 Bungeni, jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso, pamoja na mambo mengine amesema kuwa uwepo wa Bajeti kubwa katika Bodi hiyo kutaifanya kutotegemea ruzuku kutoka Serikalini.

“Mnapaswa sasa kutanua shughuli zenu ili muweze kupata kipato cha kutosha na muweze kufanikiwa kwa malengo yenu mliojiwekea, haipendezi mpaka sasa muwe mnategemea ruzuku ya Serikali, uwezo wa kujiendesha wenyewe mnao”, amesema Kakoso.

Aidha, amesisitiza Bodi hiyo kujitangaza ili iweze kufahamika na kuweza kujipatia fursa ya kupata miradi mbambali nchini itakayoweza kuleta tija kwa Bodi hiyo na Taifa kwa ujumla.

Ameelekeza Bodi hiyo kushirikiana na Halmashauri za Miji na Wilaya kuhusu usimamzi wa miradi kwani Serikali imekuwa ikipeleka miradi mingi na fedha katika Halmashauri hizo ili Bodi iweze fursa ya kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Eng. Godfrey Kasekenya amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24 Bodi imepanga kukagua jumla ya miradi 2,860 katika mikoa 26 ya Tanzania Bara, ikijumuisha miradi inayojengwa na mipya.

Amebainisha kuwa ukaguzi huo hufanyika kuhakikisha wataalamu wa majenzi wanatumika kubuni na kusimamia kwa lengo la kulinda ubora wa majengo na usalama wa raia na mali zao.

“Katika kipindi cha Julai hadi Oktoba 2023   Bodi imefanikiwa kukagua miradi 1,085 sawa na asilimia 38 ya lengo waliojiwekea na pia kusajili miradi 370 katika Ofisi za Kanda Tano sawa na asilimia 26.4 ya lengo”, amesema Kasekenya.

Kasekenya ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais  Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kufadhili mafunzo kwa vitendo kwa wahitimu wa vyuo vikuu ambapo ufadhili huo utaiwezesha Bodi kuendelea kuimarika, kuboresha utendaji kazi na kuongeza kwa idadi ya usajili wa wataalamu wa fani hiyo.

Naye, Msajili wa AQRB, Arch. Edwin Nnunduma, ametaja changamoto zinazokabili Bodi hiyo ikiwemo baadhi ya wataalamu kutokusajili miradi ya majenzi kama sheria Na. 4 ya mwaka 2010 ya Bodi inavyelekeza na hivyo Bodi kupoteza mapato kupitia miradi hiyo.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu leo imepokea Taarifa ya Utendaji wa AQRB kwa kipindi cha Julai - Oktoba 2023 iliyowasilishwa na Naibu Waziri wa Ujenzi Eng. Godfrey Kasekenya kwa niaba ya Waziri wa Wizara hiyo Mheshimiwa Innocent Bashungwa.