Habari
WIZARA YA UJENZI, TANROADS YAPANDA MITI ‘RING ROAD’ DODOMA

Wizara ya Ujenzi, kupitia Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imeendesha zoezi la upandaji miti 150 katika barabara ya mzunguko wa nje wa jiji la Dodoma ili kuadhimisha siku ya mazingira duniani 2025.
Akizungumza leo, Juni 4, 2025 kwa niaba ya Mkuu wa Kitengo cha Usalama na Mazingira kutoka Wizara hiyo, Mhandisi Mkuu, Chacha Harun amesema kuwa lengo la kupanda miti hiyo ni kuunga mkono juhudi za Serikali za kukijanisha jiji la Dodoma na kuwa jiji la mfano linalotunza mazingira.
“Mradi huu ni muhimu sana katika kutunza mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameelezwa katika Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kifungu cha 75, Sera ya Taifa ya Mazingira ya Mwaka 2021 na Mkataba wa Paris wa mwaka 2015 kuhusu mabadiliko ya tabianchi ambao Tanzania imeridhia”, amesema Mhandisi Chacha.
Aidha, Mhandisi Chacha ameeleza kuwa Wizara kupitia TANROADS itahakikisha kuwa utekelezaji wa miradi ya barabara na madaraja inahusisha upandaji wa miti ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi, kupendezesha mandhari ya Barabara na kivuli kwa watembea kwa miguu.
Kwa upande wake, Meneja Mazingira na Jamii kutoka TANROADS, Bi. Zafarani Madayi amesema kuwa, TANROADS imeshiriki kwenye maadhimisho ya Mazingira Duniani kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za TANROADS na usimamizi wa mazingira katika miradi yake.
Bi. Madayi amefafanua kuwa TANROADS imeweza kupanda jumla ya miti 150 katika barabara ya mzunguko wa Dodoma na kufanya usafi wa mazingira kama sehemu ya maadhimisho na utekelezaji wa mpango mkakati wa kupanda zaidi ya miti 40,000 kila mwaka.
Ameeleza kuwa miti 150 imepandwa katika eneo la Veyula kandokando ya barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma ambapo kuna mradi mkubwa wa upandaji miti unaoendelea sasa wa kukijanisha barabara hiyo ambao unatekelezwa na TANROADS kupitia Jeshi la Kujenga Taifa Kikosi cha Makutupora kwa kufadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Naye, Operesheni Kamanda wa zoezi la upandaji miti kutoka JKT Makutupora, Kapteni Kosa Mwangupili amesema kuwa, mradi wa upandaji miti katika barabara ya Mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma ulianza mwezi Novemba mwaka 2023 kuanzia sehemu ya Nala hadi Mahomanyika kwa kuanza na Kilomita 20 ambapo miche 18,000 ya miti ya vivuli na matunda ilipandwa.
Ameongeza kuwa zoezi hilo bado linaendelea ambapo mpaka sasa tayari wamepanda miti 36,000 kutoka Veyula hadi mji wa Serikali Mtumba.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya mazingira Duniani kitakua tarehe 05 Juni, 2025 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma ambapo yataongozwa na kauli mbiu isemayo “Mazingira yetu na Tanzania ijayo, Tuwajibike sasa: Dhibiti matumizi ya Plastiki”