Habari
TANROADS, TAA SHIRIKIANENI MIRADI YA KIMKAKATI IKAMILIKE KWA WAKATI

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ameziagiza Taasisi ya Wakala wa Barabara (TANROADS) na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA) kushirikiana na kufanya kazi kwa pamoja kumsimamia Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa jengo la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ili mradi huo ukamilike kwa wakati na ubora.
Amesisitiza Taasisi hizo kuwa na mawasiliano na ushirikiano wa karibu kwani Watanzania wanasubiria mradi huo na kuahidi yeye pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kuukagua mradi huo mara kwa mara.
Ulega ametoa maelekezo hayo Mkoani Dodoma mara baada ya kukagua utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati ambao umefika asilimia 53.9 na kusisitiza kuwa ukikamilika unatarajiwa kuinua uchumi wa Mkoa wa Dodoma na kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji.
"Nimekagua jengo hili la abiria ambalo ni la kisasa na Mkandarasi yupo nyuma ya muda, hivyo nimeagiza Mkandarasi Beijing Construction Engineering Group na Hebei Construction Group Corporation (BCEG) afanye kazi usiku na mchana na kuongeza idadi ya wafanyakazi", amesema Ulega.
Ameongeza kuwa Serikali haitaongeza muda kwa Mkandarasi huyo kama atashindwa kukamilisha ujenzi wa jengo hilo kwa wakati na atapaswa kuilipa Serikali fidia kwa kuchelewesha mradi.
"Nimetoa maelekezo kwa miradi yote Makandarasi wanapochelewesha miradi ambayo tuna uhakika tunayo fedha lazima tuwadai fidia", amesisitiza Ulega.
Waziri Ulega ameridhishwa na hatua za ujenzi wa barabara ya kuruka na kutua ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambayo imefikia asilimia 89 na kupongeza TANROADS na Mkandarasi Sinohydro kwa hatua hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuufungua mkoa huo kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa kiwanja hicho ambapo amesema uwepo wake ni fursa ya kijamii na kiuchumi kwa wana Dodoma na nchi kwa ujumla.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo amesema kuwa wanatarajia kuanza majaribio ya kuruhusu urukaji na utuaji wa ndege katika kiwanja hicho ifikapo mwezi Juni, 2025.