Habari
TANROADS MWANZA YATOA ANGALIZO KWA WAVAMIZI WA BARABARA

Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mwanza imetoa angalizo kwa wakazi wa maeneo mbalimbali wanaofanya shughuli mbalimbali zikiwemo biashara katika maeneo ya hifadhi ya barabara, kuhakikisha wanafuata taratibu bila kuvunja sheria.
Meneja wa TANROADS Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal amesema sheria namba 13 ya mwaka 2017 inakataza mtu yeyote kufanya shughuli za biashara, kulima au kujenga majengo ya makazi au biashara kwenye hifadhi ya barabara, kwani eneo hilo limetengwa kwa ajili ya matumizi ya baadae wakati wa kipindi cha matengenezo, uboreshaji na upanuzi wa barabara au ujenzi mzima wa barabara husika.
Mha. Ambrose amesema kuwa kwa sasa Serikali inampango wa kufanya upanuzi wa njia nne wa barabara ya kutoka mjini hadi Usagara, hivyo eneo litakalotumika katika upanuzi ni hifadhi ya barabara, na atakayekuwa amejenga au kufanya shughuli mbalimbali atatakiwa kuondoka na wakati mwingine kuvunjiwa.
Amesema kuwa eneo la hifadhi ya barabara ambalo ni mita 30 kila upande kutoka katikati ya barabara linaruhusiwa kwa masharti na vibali maalum , ambavyo vinatolewa na TANROADS pekee kwenye mkoa husika, na sio mamlaka nyingine.
Hatahivyo, ametoa wito kwa jamii na viongozi mbalimbali kuisaidia Serikali kwa kuwa barabara zinajengwa kwa gharama kubwa, hivyo wanapoona yeyote anafanya shughuli kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara wamzuie, au kutoa taarifa TANROADS, au kupeleka taarifa kwa viongozi mbalimbali wa mkoa, wilaya, tarafa na kata, ili waweze kuelimishwa madhara ya kuvamia hifadhi ya barabara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mtaa wa Mitimirefu Buhongwa, Bw. Phracedic Thomas amesema wananchi wanaofanya shughuli mbalimbali kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara, wengi wao hawatambui kufanya hivyo ni kosa na hawana vibali maalum, hivyo ameomba elimu itolewe mara kwa mara.
Naye, Mwenyekiti wa kituo cha bodaboda cha Buhongwa C, Bw.Carles Komanya ‘Makassi’, amesema wafanyabiashara wahakikishe wanapata vibali sehemu maalum inayohusika na vibali na sio kuchukua vibali sehemu nyingine yeyote, ili kuepusha mgongano.
Amesema athari kubwa wanayoweza kupata kwa kuweka bodaboda eneo la barabarani n ipamoja na kupata ajali, hivyo ametoa rai kwa serikali kutambua bodaboda wanatoa huduma kwa jamii hivyo isaidie wapate sehemu salama kwa ajili ya kutoa huduma zao.
Kategere Simon, ambaye ni dereva wa bodaboda amesema wafanyabiashara wengi waliopo barabarani wanasababisha msongamano na foleni za magari kutokana na kuweka biashara zao na kumega sehemu kubwa ya barabara, halikadhalika daladala zinazoingia kituo cha daladala cha Buhongwa zimekuwa zikikaa muda mrefu badala ya kupakia au kushusha na kuondoka, nazo zinachangia msongamano wa watu na magari mengine kwenye barabara kuu.