Habari
SERIKALI KUJENGA BARABARA YA NJIA NNE MWANZA.

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imejipanga kikamilifu kuleta mapinduzi ya miundombinu katika Jiji la Mwanza kupitia ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Mwanza Mjini hadi Usagara pamoja na njia ya mabasi ya mwendokasi, hatua inayolenga kufungua fursa mpya za kiuchumi kwa jiji hilo na mikoa jirani.
Akizungumza kuhusu mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Ambrose Pascal amesema kuwa maandalizi ya ujenzi yamekamilika na utekelezaji utaanza mara tu baada ya kumpata Mkandarasi mshindi wa zabuni iliyotangazwa.
“Barabara hii itakuwa ya njia nne na katikati yake tutaweka njia ya mwendokasi kwa ajili ya matumizi ya baadaye. Hii ni sehemu ya mpango mpana wa Serikali wa kupunguza msongamano mkubwa wa magari katika barabara ya Mwanza Mjini hadi Usagara”, alisema Mhandisi Pascal.
Aidha, Mhandisi Pascal amebainisha kuwa Serikali kupitia Mfuko wa Serikali Kuu inaendelea kugharamia miradi mingine muhimu ya barabara, ikiwemo ujenzi wa Daraja la Simiyu lililopo umbali wa kilomita 65 kutoka Mwanza mjini na kilomita 3 kutoka Magu ambapo Mkandaraisianayetekeleza daraja hilo ni Daraja kampuni ya CCECC kwa gharama ya Shilingi Bilioni 48, na utekelezaji wake umefikia asilimia 60 na linatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba 30, 2025.
Ameongeza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa Daraja hilo la Simiyu lenye urefu wa mita 175 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 3 utarahisisha shughuli za usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na Mikoa jirani ya Mara na Simiyu kwa kuwa katika daraja hilo litaweza kupitisha magari mawili kwa wakati mmoja tofauti na hivi sasa magari yanapita kwa zamu upande mmoja.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Paschal ameeleza kuwa TANROADS inaendelea na ujenzi wa Daraja la Sukuma lenye urefu wa mita 70 na barabara unganishi zenye urefu wa kilomita 2.3 ambalo linatekelezwa na Mkandarasi Mzawa Mumangi Construction kwa gharama ya Shilingi Bilioni 9.78 na hadi sasa ujenzi wake umefikia asilimia 60 na mradi huo unatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba , 2025.
Mhandisi Pascal amesisitiza kuwa miradi hiyo mikubwa ya uboreshaji wa miundombinu ya upanuzi wa barabara na madaraja italeta tija kubwa kwa uchumi wa wakazi wa Mwanza na maeneo jirani.
“Uboreshaji huu utapunguza muda wa safari na kupunguza gharama za usafirishaji wa watu na bidhaa, hivyo kuinua shughuli za kibiashara”, ameeleza Mhandisi Paschal.