...
MAFUNDI SANIFU (TEMESA) WAFUNDWA KUHUSU USIMAMIZI NA UKAGUZI WA MAZINGIRA, MOROGORO.
Habari
Matukio
MAFUNDI SANIFU (TEMESA) WAFUNDWA KUHUSU USIMAMIZI NA UKAGUZI WA MAZINGIRA, MOROGORO.

Mafundi sanifu wa Wakala wa Umeme na Ufundi (TEMESA), kutoka mikoa mbalimbali nchini wameaswa juu ya umuhimu wa tathmini, usimamizi na ukaguzi wa mazingira  yao ya kazi ili kuweza kudhibiti athari za mazingira zinazowakabili na kusababisha mabadiliko ya tabia nchi.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Idara ya Tathmini ya Athari ya Mazingira kutoka Baraza la Taifa la kuhifadhi Mazingira (NEMC), Eng. Ignance Mchallo wakati wa mafunzo ya tathmini na usimamizi wa mazingira kwa mafundi sanifu yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Aidha amewataka mafundi hao kutumia sheria ya mazingira ya mwaka 2004 kwa kuwa sheria hiyo si tu kulinda haki peke yake bali pia kuondoa vikwazo, kutoa mwongozo wa utendaji na kupunguza mzigo wa kiutendaji, pamoja na kuboresha uwajibikaji na ufanisi kwa ajili ya maendeleo endelevu ya nchi.

“Sheria ya mazingira ni sheria mama ya mazingira na yenye nguvu katika utekelezaji, na pia inaweza ikawa juu ya sheria nyingine pindi matatizo yanapojitokeza. Ni haki kwa kila mtu kuishi katika mazingira salama na safi, endapo mazingira yakaharibiwa unayo haki ya kuitumia sheria hii kwa kushtaki ukiukwaji wa utunzaji wa mazingira eneo husika”, alisisitiza Mkurugenzi Mchallo.

Mkurugenzi Mchallo aliongezea kuwa Sheria ya mazingira inahitajika kuzingatiwa na kutekelezwa na watu wote hususan wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi ili kuhakikisha wanaboresha afya zao na kuweza kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi, Eng. Melania Sangeu amewataka mafundi sanifu hao kuzingatia mafunzo hayo na kutathimini mazingira katika maeneo wanayofanyia kazi kwa kuwa lengo ni kujenga uelewa wa masuala ya mazingira pamoja na mbinu za kufanya tathmini ya mazingira na utekelezaji wake.

“Mazingira salama ndiyo chachu ya ufanisi mzuri wa kazi, hivyo basi maeneo yenu ya kazi yawe katika mazingira safi kwa kufuata utunzaji mzuri wa mazingira unaotakiwa pamoja na kutengwa maeneo sahihi ya kumwaga mafuta machafu ya magari, maeneo ya kuchomea taka, mpangilio mzuri wa vifaa vya kufanyia kazi, na kuwa na vifaa vya kutosha vya usalama pamoja na kufahamu namna na wakati wa kuvitumia”, alisema Eng. Sangeu.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Taasisi ya Ufundi Dar es Salaam (DIT), Eng. Kinyawa Kirama ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa jitihada zake za kutambua umuhimu wa mazingira ambapo amesema kupitia mafunzo hayo mafundi sanifu hao watakuwa mfano kwa wengine katika masuala ya usimamizi na utunzaji wa mazingira katika maeneo yao ya kazi.